advanced Search
KAGUA
9309
Tarehe ya kuingizwa: 2010/09/28
Summary Maswali
hivi ni kwa nini Imamu Ali (a.s), hakuamua kilinda nafsi yake mbele ya adui yake (Ibnu Muljim), hali ya kuwa Yeye (a.s) alikuwa akielewa vyema nia ya adui huyo?
SWALI
sote tunaelewa kuwa: Imamu Husein alisimama kidete mbele ya maadui zake, Naye (a.s) alisimama mbele ya mashetani hao huku akiwatolea dalili mbali mbali kwa ajili ya kuitetea haki pamoja na nafsi yake. Lakini kwa upande wa Imamu Ali (a.s), sisi hatukuona aina yoyote ile ya Yeye (a.s) kujitetea au kuchukua aina fulani ya tahadhari kwa ajili ya nafsi yake, huku Yeye (a.s) akiwa ni mwenye kuifahamu vyema nia mbaya ya adui yake ilivyo, huku Yeye (a.s) akionekana tokea mwanzo wa usiku kujitayarisha vyema kwa ajili ya kwenda kwenye mauti ya muhanga yaliyokuwa yakimsubiri msikitini. Vile vile tusisahau kuwa Yeye (a.s) alifanya hivyo huku akiwa na dalili madhubuti iliyofungamana na elimu ya yakini, labda pengine sisi bado hatujaweza kuifahamu dalili na hoja kuhusiana na hilo. Kwa kutokana na hilo mimi ninasubiri jawabu zenu kuhusiana na swali langu.
MUKHTASARI WA JAWABU

Jawabu kamili ya swali hili yaweza kukamilika kuvitambua vipengele vifuatavyo:

  1. Vigezo halisi kwa mja katika utendaji wa amali na nyadhifa zake zinazomfungamanisha na wanajamii mbali mbali, ni ile elimu yake ya kawaida.

Imamu (a.s) huwa hatumii nguvu zake za ndani zinazotokana na utukufu wa roho yake ambazo ni zenye kushikamana na ulimwengu wa Ghaibu katika kukabiliana na wengine, bali Imamu (a.s) hukabiliana na watu mbali mbali kupitia hali dhahiri ya mambo yalivyo, na kama yeye maishani mwake atakuwa daima ni mwenye kutumia kipaji chake, au kwa lugha nyengine, atakuwa ni mwenye kukabiliana na watu kimatendo kupitia nguvu za Ghaibu, hapo watu watatengana naye, kwani watu hawawezi kukabiliana na nguvu za Ghaibu maishani mwao.

  1. Ulimwengu huu ni ulimwengu wa mitihani na majaribio. Kwa hiyo ili mtu atumbukie kisawa sawa ndani ya ulimwengo wa majaribio, ni lazima atende matendo yake ya kijamii kupitia elimu ya dhahiri, na iwapo Mtume au Imamu (a.s) ataiangalia jamii na wanajamii na kutenda matendo yake kupitia jicho la Ghaibu, hapo yeye atakuwa tayari ameshatengana na ulimwengu huu wa majaribio. Hii ni kwa kutokana na kuwa katika hali kama hiyo yeye atakuwa ni kizuizi cha kuwazuia wengine wasitende matendo yao kwa hiari zao na kwa uhuru kamili wa nasfi zao.

Kwa ibara nyengine ni kwamba: ni kweli kwamba kila mmoja ana wadhifa wa kuitetea nafsi yake, lakini utetezi huu unatakiwa kufanywa kupitia misingi ya elimu ya kawaida, na wala mtu hatakiwi kuwazuia wengine wasiyafanye wayatakayo kupitia nguvu za Ghaibu. La pili ni kwamba: Ibnu Muljim ndiye aliyekuwa akitahiniwa katika tokeo hili la kuuliwa kwa Imamu Ali (a.s), kwa hiyo Imamu Ali (a.s) hakutakiwa kuyazuia matakwa ya Ibnu Muljim, huku yeye alikuwa ndani ya uwanja wa mitihani, na iwapo Imamu Ali (a.s) angelitumia jicho lake la Ghaibu kwa ajili ya kukabiliana na Ibnu Muljim, hapo angelimfanya Ibnu Muljim kuwa ni mtu aliyelazimika kutotenda matendo yake kwa hiari yake.

JAWABU KWA UFAFANUZI

Pale Imamu au Mtume (a.s) anapotenda matendo yake yanayofungamana na haki za wanajamii wenzake, huyatenda matendo hayo kupitia msingi wa elimu ya dhahiri yenye kudirikiwa na kuzingatiwa watu wa kawaida, na ni kawaida ya Maimamu na Mitume (a.s) kumuabudu Mola kama vile Wao walivyowafundisha wengi kumuabudu Mola huyo, kwani sheria za dini huwa zinawafunga wanajamii wote katika mtindo mmoja, na wala wao hawatakiwi kutafautiana katika hilo. Kwa hivyo Mitume na Maimamu huwahukumu na kuwaendesha wanajamii wa jamii zao kupitia sheria moja zenye aina moja ya mfumo wa hali dhahiri ya mambo yanavyoonekana, wala wao hawawahukumu watu kupitia elimu ya Ghaibu. Kuhusina na hilo hebu ianglie Riwaya ifuatayo:

(قَالَ رَسُولُ اللَّهِ ص إِنَّمَا أَقْضِي بَيْنَكُمْ بِالْبَيِّنَاتِ وَ الْأَيْمَانِ وَ بَعْضُكُمْ أَلْحَنُ بِحُجَّتِهِ مِنْ بَعْضٍ فَأَيُّمَا رَجُلٍ قَطَعْتُ لَهُ مِنْ مَالِ أَخِيهِ شَيْئاً فَإِنَّمَا قَطَعْتُ لَهُ بِهِ قِطْعَةً مِنَ النَّارِ.)

 Maana yake ni kwamba: Mtume (s.a.w.w) amesema: (Kwa hakika mimi ninatoa hukumu mbali mbali zenye mzozo katika jamii kupitia bayana za mashahidi zinazobainishwa mbele yangu, au viapo vyenu juu ya madai yenu, na miongoni mwenu mna watu wenye nguvu za ufasaha na maneno madhubuti katika ujengaji wa hoja na dalili juu ya madai yao kuliko wengine, hivyo basi eleweni kwamba: yeyote yule nitakayemkatia sehemu ya mali ya nduguye (kwa kutokana na nduguye kutokuwa na uwezo wa kuwa na nguvu upangaji wa maneno katika kuitetea haki yake) huyo anatakiwa kutambua kuwa mimi nimemkatia kipande cha moto.)[1]

Maana ya Riwaya hii ni kwamba Mtume huhukumu kupitia hali dhahiri ya mambo yalivyo, na kwa jinsi ushahidi unavyoonesha, kwa hiyo iwapo mtu atakula kiapo kwa ajili ya kutaka kumdhulumu mwenziwe pamoja na kusimamisha dalili juu ya hilo, na dalili hizo zikaweza kidhahiri kuonekana kuwa ni dalili madhubuti, hapo mimi nitakuwa sina budi kupitisha hukumu zangu kwa mujibu wa dalili hizo zilivyo, na kwa kuwa kila mmoja anatambua vilivyo juu ya haki anayoidai kuwa ni yake au sio yake, hivyo basi ni lazima kila mmoja awe makini katika kuepukana na uongo wenye nia ya kuwadhulumu wengine. Na iwapo mtu atatunga uwongo kwa ajili ya kuila haki ya nduguye, basi afahamu kuwa atakuwa anakula moto.

Ingawaje basi Imamu Ali (a.s) alikuwa akijua nia ya adui wake ilivyo, lakini Yeye (a.s) hakuwa na haki ya kutumia elimu yake ya ndani iliyofungamana na ulimwengu wa Ghaibu, ili kujitetea au kumhukumu Ibnu Muljim, kwani Yeye (a.s) alikuwa ni kigezo kwa wanajamii wa jamii anayoiongoza, kwa hiyo Yeye (a.s) aliwajibika kuishi na watu kwa jinsi ya dhahiri ya mambo yalivyo, kwani hiyo ndiyo njia inayodirikiwa na kuzingatiwa na walimwengu wa kawaida, kwa hiyo nyenendo na tabia zake mbele ya wanajamii, zilihitajia kuenda sawa na jicho la elimu ya dhahiri linavyo yazingatia mambo mbali mbali katika mtizamo wake. Maimamu na Mitume (a.s) hawakuwa wakiyaangalia mambo kwa jicho la Ghaibu isipokuwa baadhi ya wakati tu, na hilo huwa linahitajia amri kutoka kwa Mola Mtukufu.

Pia tusisahau kuwa ulimwengu huu ni uwanja wa mitihani, na mfumo wake wenye kufuata njia maalumu za kimitihani. Qur-ani kuhusiana na hilo inasema: (Hivi watu wanadhania kuwa sisi tutawaachia tu pale wanaposema tumeamini, bila sisi kuwatia mitihanini)?[2] Na katika Aya nyengine Mola anasema: (Yeye (Mola) ndiye aliyeumba uhai na mauti ili akujaribuni ni nani mwenye amali njema zaidi miongoni mwenu.)[3] Ili mtu atahiniwe, ni lazima kwanza ihakikishwe kuwa yeye ni mwenye uwezo na uhuru kamili juu ya lile analotahiniwa nalo, na hapo ndipo yeye atapostahiki kupata malipo juu ya matendo yake. Hali ya kuwa iwapo Mitume na Maimamu (a.s) watatumia elimu yao yenye kufungamana na ulimwengu wa Ghaibu katika kukabiliana na mambo mbali mbali, hilo litakuwa ni kizuizi kitakachowanyima wengine uhuru juu ya utendaji wa matendo yao.

Ni kweli kwamba Imamu Ali (a.s) ana wajibu wa kuihifadhi nafsi yake ipaswavyo, lakini wadhifa huu unatakiwa kutekelezwa kupitia elimu ya dhahiri inavyo onesha, na wale Yeye (a.s) hatakiwi kutumia nguvu za Ghaibu katika kuitetea nafsi yake au katika kuwahukumu wanajamii mbali mbali. Jengine linalopaswa kuzingaitiwa hapa ni kwamba: kuuwawa kwa Imamu Ali (a.s), kulikuwa kukifungamana moja kwa moja na lile tendo la Ibnu Muljim, tendo ambalo lilikuwa likibebwa ndani ya nia mbaya iliyomo ndani ya nafsi ya mtu huyo, naye kwa kweli alikuwa katika uwanja wa kutahiniwa, kwa hiyo ili yeye aweze kutahinika kisawa sawa, ni lazima awe na uwezo na hiari kamili juu ya lile analotaka kutahiniwa nalo, kwa hiyo hakutakiwi kutumia nguvu fulani zitakazomtoa yeye katika uwanja huo, huku tukizingatia kuwa, miongoni mwa masharti ya kutahiniwa, ni mtu kuwa na nguvu pamoja na hiyari za kutenda yale matendo anayotahiniwa nayo. Basi Imamu Ali (a.s) hakutumia nguvu za Ghaibu katika kujitetea, ili ampe yeye nguvu na uhuru kamili wa kuamua kati ya kutenda au kuto tenda yale anayoamarishwa na shetani kuyatenda. Na hili la watu kutakiwa wawe huru katika matendo yao, ni miongoni mwa matakwa ya Mola yenye kushikamana na njia madhubuti za kuwatahini waja wake, jambo ambalo Mola ameliamua kumvaa kila mmoja wetu huku yeye akiwa huru mwenye hiari kamili, na huo ndio mfumo wa Mola usiobadilika. Mola kuhusiana na hilo amesema: (Wala hamtokuta mabadiliko kwenye mfumo wa Mola)[4].


[1] Al-Kafi, juz/7, uk/414, mlango wa sheria za kimahakama.

[2] Suratu Ankabuut, Aya ya pili.

[3] Suratul-Mulki Aya ya pili.

[4] Suratu Faatir, Aya ya 43.

 

TARJAMA YA JAWABU KATIKA LUGHA NYENGINE
MAONI
Idadi ya maoni 0
Tafadhali ingiza thamani
mfano : Yourname@YourDomane.ext
Tafadhali ingiza thamani
<< Niburute.
Tafadhali ingiza kiasi sahihi ya usalama Kanuni

MPANGILIO WA KIMAUDHUI

MASWALI KIHOLELA

YALIYOSOMWA ZAIDI